Homa ya mapafu ni aina ya maambukizi yanayoathiri mapafu. Ni ugonjwa ambao unaua watoto wengi hasa katika nchi zinazoendelea duniani.
Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio chini ya miaka 5 wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.
Kutokana na vifo vingi vinavyotokana na homa ya mapafu tarehe 12 ya mwezi wa Novemba kila mwaka imefanywa kuwa siku rasmi ya homa ya mapafu duniani, ambapo nembo ya siku hiyo ni nguo za rangi ya bluu.
Muundo wa Mapafu
Mapafu yanajumuisha mirija mikubwa ya hewa (bronchi) ambayo hugawanyika kufanya mirija midogo zaidi ya hewa (bronchioles), ambayo nayo hutengeneza vifuko vidogo vidogo ya hewa (alveoli). Vifuko hivi vidogo vya hewa (alveoli) vina mishipa ya kupitisha damu (capillaries) ambayo husaidia kuchuja na kusafirisha hewa safi ya oksijeni tunayovuta kuingia kwenye damu na hewa chafu ya ukaa (kaboni dioksidi) kuondolewa kwenye damu na kuingizwa kwenye mapafu tayari kwa kutolewa nje ya mwili.
Kwa kawaida vifuko hivi vidogo hujaa hewa muda wote tayari kwa kusafirishwa. Inapotokea mtu akapata homa ya mapafu, vifuko hivi hujaa maji au usaha hivyo kuathiri upitishaji wa hewa safi kwenye damu na kusababisha tatizo la kupumua.
Homa ya mapafu husababishwa na nini?
Kuna aina kadhaa ya vimelea ambao vinaweza kusababisha maambukizi ya mapafu. Vimelea hivi hujumuisha bakteria, virusi, parasite na fangasi.
Vimelea hawa hushambulia mwili wa binadamu kulingana na umri na kinga ya mwili. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa watoto wakubwa.
Baadhi ya vimelea wa bakteria wanaoshambulia watoto ni pamoja na Streptococcus pneumoniae ambao ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.
Wapo pia Haemophilus influenzae aina b (Hib) ambao ni aina ya pili ya bacteria walio maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa mapafu kwa watoto. Staphylococcus aureus ni aina nyingine ya bacteria ambao hushambulia zaidi watoto wachanga.
Kuna pia Group B streptococci ambao pia hushambulia zaidi watoto wachanga.
Kwa upande wa virusi, virusi wa aina ya Respiratory syncytial virus ndiyo wanaoongoza kwa kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.
Aidha, vimelea wa Pneumocystis jiroveci ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasite ni maarufu zaidi miongoni mwa parasite wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini hususani watoto wenye VVU.
Aina nyingine za bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na Mycoplasma pneumonia naChlamydia pneumonia.
Jinsi Homa ya Mapafu inavyoenezwa
Kuna namna nyingi za kuenea kwa homa ya mapafu. Kwa kawaida, virusi na bacteria hupatikana katika sehemu ya juu ya mfumo wa njia ya upumuaji (upper respiratory tract).
Inapotokea kinga ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yeyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji (lower respiratory tract) na hatimaye kushambulia mapafu. Hali kadhalika, vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya kuzaliwa yaani kipindi cha mimba.
Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu
Dalili za vichomi au homa ya mapafu kwa watoto hutegemea na umri wa mtoto. Kwa watoto wadogo,
dalili za awali zinaweza kuwa:
homa kali pamoja na mtoto kuhangaika na kunyong'onyea.
Watoto wanaozaliwa wakiwa na uambukizi wa bacteria aina ya Streptococcus kundi B wanaweza kuwa na homa na kupumua kwa shida.
Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na dalili ambazo si maalum (no-specific symptoms) kama vile kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yeyote ya kushindwa kupumua.
Hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.
Dalili za kawaida za homa ya mapafu ambazo huwapata karibu watoto wote wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja na:
homa
Kuhisi baridi ,kikohozi
Kupumua kwa haraka kuliko kawaida
kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa kupumua, Mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa kupumua, maumivu ya tumbo, kupoteza hamu ya kucheza, kupoteza hamu ya kula na kushindwa kunyonya, Mtoto kubadilika rangi na kuwa na rangi bluu katika midomo na kucha
Hata hivyo, si lazima dalili zote hizi ziwepo kwa kila mtoto.
Baadhi ya watoto huonesha kupumua kwa haraka kama dalili pekee ya homa ya mapafu.
Iwapo vimelea vimeshambulia sehemu za chini ya mapafu karibu ya tumbo, sehemu ijulikanayo kama kiwambo au diaphragm, mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya kushindwa kupumua ingawa anaweza kuwa na homa na kujihisi maumivu makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika.
Watoto wachanga wanaweza kushindwa kunyonya, na pia kupoteza fahamu na kupata degedege.
Vihatarishi vya homa ya mapafu (risk factors)
Katika hali ya kawaida kinga ya mtoto mwenye afya njema humlinda asishambuliwe na vimelea vinavyosababisha magonjwa mbalimbali. Hali huwa ni tofauti pale ambapo kinga ya mtoto ni ndogo au dhaifu, kwa vile mfumo mzima wa ulinzi huathirika na hivyo basi inakuwa ni rahisi kwa mtoto kupata homa ya mapafu.
Mfumo wa kinga wa mtoto unaweza kuwa dhaifu kwa ukosefu wa lishe bora hasa kwa watoto wachanga ambao hawanyonyeshwi ipasavyo.
Aidha uwepo wa magonjwa mengine, kwa mfano, maambukizi ya VVU, saratani na ugonjwa wa Surua hupelekea kinga ya mwili kuwa dhaifu.
Lakini vile vile kuna mazingira yanayoweza kusababisha mtoto kuwa katika hatari ya kupata homa ya mapafu mfano moshi wa sigara, au moshi ndani ya nyumba unaosababishwa na kupikia kuni au mkaa.
Vilevile msongamano ndani ya nyumba kutokana na watu kuwa wengi sehemu moja nayo huweza kusababisha watoto kupata homa ya mapafu.
Uchunguzi na Vipimo
Daktari humchunguza mtoto mgonjwa kwa kusikiliza dalili za ugonjwa kutoka kwa mzazi/mlezi wa mtoto, kuchunguza viashiria vya ugonjwa huu na kisha kumpima mtoto kwa kutumia kifaa kinachosaidia kusikia sauti mbalimbali katika mfumo wa hewa wa mgonjwa kiitwacho stethoscope.
Ili kujiridhisha na kuwa na uhakika wa tatizo hili, vipimo vifuatavyo vinaweza kufanywa kulingana na mazingira na upatikanaji wake. Vipimo hivyo ni pamoja na X-ray ya kifua, au CT-scan ya kifua, pamoja na damu ili kuchunguza madhara yaliyoletwa na homa hii ya mapafu.
Faida ya kipimo cha CT-scan ni ule uwezo wake wa kutofautisha aina tofauti za homa ya mapafu na aina ijulikanayo kama Atypical pneumonia ambayo si rahisi kuonekana kwa kutumia X-ray ya kawaida ya kifua. X-ray ya kifua na CT-scan ya kifua kwa pamoja vina uwezo wa kuonesha tatizo hata pale ambapo daktari ameshindwa kusikia sauti maalum kwa kutumia kifaa chake cha stethoscope.
Matibabu
Maamuzi ya Matibabu kwa watoto wenye homa ya mapafu hutegemea aina ya vimelea, umri na hali ya mtoto. Mara nyingi antibiotics ndizo hutumika katika kutibu homa ya mapafu inayosababishwa na maambukizi ya bakteria. Kwa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi, antibiotics hazina uwezo wowote wa kutibu.
Ieleweke kuwa ni tabibu anayeweza kufahamu kama mtoto wako anahitaji antibiotics au dawa za aina nyingine, kwahiyo ni muhimu kwa mzazi ama mlezi kumpeleka mtoto hospitalini haraka pindi mtoto anapoonesha dalili za ugonjwa huu badala ya kuamua kumpa dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Namna ya kuzuia Homa ya mapafu
Homa ya mapafu inaweza kuzuiwa kwa chanjo, lishe bora na ya kutosha na mtoto kuishi katika mazingira yenye hewa safi.
Kuzuia homa ya mapafu kwa watoto ni sehemu muhimu ya mkakati wa Taifa wa kupunguza vifo vya watoto. Chanjo dhidi ya Hib, pneumococcus, surua na kifaduro ni njia mojawapo ya kuzuia homa ya mapafu.
Lishe ya kutosha ni muhimu kwa kuboresha kinga ya mwili ya mtoto ambapo inashauriwa mama kunyonyesha mtoto bila kuchanganya na kitu chochote walau kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha yake.
Kuhimiza usafi katika makazi kama kutotumia jiko la mkaa au kuni ndani ya nyumba na uvutaji wa sigara ni jambo linaloshauriwa pia. Hii inasaidia kupunguza idadi ya watoto kupata homa ya mapafu. Kwa watoto wenye VVU, matumizi ya dawa ya cotrimoxazole kila siku husaidia kupunguza uwezekano wa kupata homa ya mapafu.
Utafiti umeonyesha kwamba kinga na tiba sahihi ya homa ya mapafu inaweza kuzuia vifo milioni moja kwa watoto duniani kila mwaka. Hivyo ni wajibu wetu sote kushirikiana kupambana na ugonjwa huu wa homa ya mapafu